Tuesday, 10 February 2015

PITIO LA AGANO LA KALE I




Mada ya Kwanza. Utangulizi wa Pitio la Agano la Kale.
Malengo ya mada.
Baada ya kumaliza mada hii mwanafunzi ataweza:
·        Kueleza  maana ya  Agano.
·        Kueleza maana ya Biblia
·        Kueleza maana ya Agano la Kale
·        Kueleza maana ya Pitio la Agano la Kale.
·        Kutambua mpangilio wa vitabu katika Biblia ya kiebrania (Agano la kale).
·        Kutambua muundo wa Agano la Kale katika Biblia yetu ya Kiswahili na Kiingereza.
·        Kueleza kwanini wakristo wanasoma Agano la Kale.
·        Kueleza Sababu za kujifunza Kozi ya Pitio la Agano la kale.
·        Kulinganisha na kulinganua kati ya Agano la Kale na agano Jipya.
I. Utangulizi .
Somo hili linachunguza Agano la kale kwa ujumla  tu. Halilengi kujifunza kila kitu kinachotajwa katika Agsno la Kale, bali ninafanya mapitio tu na kutoa mtazamo wa jumla wa kila kitabu  na mtazamo wa jumla wa Agano la kale.
Lengo la kozi hii ni kutoa mwanga na msingi  kwa mwanafunzi juu ya Agano la Kale na kumjengea mwanafunzi uwezo na msingi mzuri  wa kulielewa Agano la Kale  na kutambua uhusiano uliopo kati ya Agano la Kale na Agano Jipya.
Katika kozi hii mwanafunzi atajifunza kila kitabu cha agano la kale kwa muhtasdasri tu kwa kutazama muuundo wa kitabu, mtindo, mafundisho makuu,  matukio makuu na, mwandishi, mwaka wa kuandikwa,watu mashuhuri, mitajo   ya Kristo na  mistari ya kiini cha kila kitabu.
Kozi hii  imegawanya katika sehemu tatu ili kurahisisha ujifunzaji na ufundishaji. Lakini kimsingi ni kozi moja.
Kila sehemu ya kozi hii itafundishwa kwa wiki moja.
II. Umuhimu wa  kujifunza pitio la Agano la kale.
1.     Linatupa ufahamu juu ya historia ya mwanadamu tangu uumbaji mpaka sasa.
2.     Linatupa ujasili wa kusimama na kuitetea imani bila kuteteleka kama walivyofany watakatifu wa Agano la Kale.
3.     Kupitia Kozi hii tunatambua kwamba Mungu wa Agano la Kale ndiye yeye Yule wa Agano Jipya.
4.     Tunajengewa msingi mzuri wa kuifahamu thiolojia ya Agano la Kale.
5.     Tunatambu ya kwamba wokovu kwa  neema kwa njia ya imani  umekuwa daima ndiyo njia ya pekee  ya kuwa na mahusiano na ushirika na Mungu.     
6.      Tunatambua ya kwamba kutembea kwa imani kumekuwa daima ndiyo njia pekee ya kumpendeza Mungu.
III. Ufafanuzi wa Istilahi.
Katika kipengele hiki tutafafanua  baadhi ya Istilahi mbalimbali kama zitakavyotumika katika kozi hii ya Pitio la Agano la Kale na kama zilivyotumika katika Biblia na elimu ya thiolojia kwa ujmla.   
Biblia. Ni neno la Mungu lililo katika maandishi. Bibblia pia ni kitabu cha mawazo na matendo ya Mungu.Biblia pia inaweza kufafanuliwa kama mkusanyiko wa maandiko matakatifu yaliyoandikwa katika vipindi mbalimbali vya historia ya mwanadamu na watu walioongozwa na Roho mtakatifu kuandika.2Pet 1:19-21. 2Tim 2:15-17.
Neno la Mungu pia hujulikana kama maandiko. Neno maandiko ni neno la kilatini ambalo humaanisha maandishi.  Wakati neno maandiko linapokuwa limetumika na kuwa na helufi kubwa mwanzoni mara nyingi humaanisha maandiko matakatifu yaani Biblia.
 Maana ya Agano. Neno agano linatokana na neno la kiebrania Berith lenye maana ya mapatano, makubaliano au mkataba unaofanywa baina ya pande mbili.
Neno hili Agano kwa Kiyunani ni Diatheke lenye maana ya urithi au wosia.
 Kwa hiyo tunaweza kusema agano ni mapatano maalumu yanayounganisha watu wa pande mbili pamoja.
Neno  Agano la Kale Hulenga hasa kwenye Agano la Musa ambalo Mungu alifanya na wana wa Israeli katika mlima Sinai Baada ya kutoka Misri   lakini kabla ya kuingia kwenye nchi ya ahadi. Kut 20-24. Kum 28-30, Yer31:32 Gal 3:6-26, Ebr 9:15-22.
Vitabu 39 vya kwanza katika Bibli vinaitwa Agano La Kale.
AGANO maana yake ni mapatano au makubaliano kati ya watu. Sehemu ya kwanza ya Biblia inaitwa "AGANO LA KALE" kwa sababu inaeleza habari ya agano (mapatano) kati ya Mungu na wanadamu wa kale.

Pia Agano la Kale ni maelezo ya Kikristo  ya vitabu vilivyotolewa na Mungu kwa watu wa kiyahudi na ambayo yanahusika na Agano la kale ambalo Mungu aliwapa Waisraeli  kwa kupitia kwa Musa kwenye mlima Sinai.
Agano la kale ni zaidi ya sheria, hutoac taarifa na historia ya elimu ya kithiolojia yaw a agano la Mungu  kulingana na mpango wake wa wokovusi kwa wayahudi pekee bali pia na kwa watu wa mataifa.
Hivyo twaweza kuhitimisha kwa kusema  kwamba Agano la kale humaanisha vitabu vyote vilivyo katika Biblia vilivyoandikwa kabla ya kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo. Au ni maandiko matakatifu yaliyoandikwa kabla ya kuzaliwa kwa Masihi  yaani Bwana wetu Yesu Kristo.
IV. Muhtasari.
1.     Agano la kale liliandikwa kwa muda wa kama miaka1000. Hivi.
2.     Liliandikwa kama  na waandishi kama  30 chini ya uongozi wa Roho mtakatifu kama mwandishi mkuu.
3.     Lina jumla ya vitabu 39.
4.     Agano la kale liliandikwa hasa kwa kiebrania na sehemu chache sana ziliandikwa kwa kiaramu.
5.     Maandiko matakatifu  ya asili yalinakiliwa kwa uangalifu  na kwa ustadi sana  kwa mkono na waandishi wa kiyahudi na kisha yakapokelewa toka kizazi hata kizazi.
6.     Wakati Bwana Yesu alipokuja ulimwenguni  alikuta Agano la kale limekkwisha kukamilika na kuwa  kitabu kimoja chenye vitabu 24 kwa kiyahudi,  tulivyonavyo leo ambavyo ni sawa na vitabu 39 katika Biblia yetu vya Agano la Kale.

7.     Tafsriri ya kwanza ya  Agano la kale ya kiyahudi ilikuwa  kwa lugha ya kiyunani ambayo iliitwa Septuaginta (LXX). Iliitwa hivyo kwa  sababu tafsiri hiyo ilifanywa na watu sabini. Na tafsriri hiyo ilikamilika mnano mwaka 250 K.K.

8.     Tafsri ya pili ambayo ilikuwa muhimu ni ile ya kilatini  iliyojulikana kama “ Latin vulgate “ (383-450 BK). Biblia hii ndiyo iliyokuwa Biblia ya Kikristo iliyotambuliwa kwa muda wa miaka  elfu moja.

9.     Tafsiri ya kwanza kwa lugha ya Kiingereza   ilifanywa mnamo mwaka 1384 na John Wicliff, na kufuatiwa na lie iliyoruhusiwa na mfame James manamo mwaka 1611. Tafsiri hii ndiyo tafsiri ya mwanzo kabisa ya karibu  tafsiri zetu zote za kisasa.
10.                        Nakala zilizopatikana kule Kumlani pwani ya Bahari mfu (Dead sea.) mnamo mwaka 1947 zilithibitisha usahihi  na muunganisho wa vitabu vyote pamoja vya Agano la Kale kama tulivyo na kitabu hicho hivi leo.
11.                        Kitabu cha Agano la Kale kimelindwa na kuhifadhiwa kiajabu na Mungu baba kwa muda wa zaidi ya  miaka elfu tatu.



V. Mpangilio wa vitabu katika Biblia ya Kiebrania.

                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                       
SHERIA
MANABII
MAANDIKO.
Mwanzo
Kutoka
Mambo ya walawi
Hesabu
Kumbukumbu la torati.
Wa kwanza
Yoshua
Waamuzi
Samweli (vitabu 2)
Wafalme(vitabu 2)

Waliofuata.
Isaya
Yeremia
Ezekieli
Manabii wadogo 12.
Ushairi.
Zaburi
Mithali
Ayubu.
Magombo matano.
Wimbo  wa Solomoni (Ulio bora).
Ruthu
Maombolezo
Mhubiri
Esta.
Historia.
Danieli
Ezra-Nehemia.
Mambo ya nyakati
(vitabu  2)

·        Utaratibu huu wa mapangilio wa vitabu wa kiebrania ndio Yesu
Alioutumia.  Luka 24”27.
 “Kisha akawaambia, haya ndiyo maneno yangu  niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, yakwamba nilazima yatimizwe yote niliyoandikiwa  katika Torati ya Musa, , na katika Manabii, na katika Zaburi”
 Wayahudi wakati wa Yesu   walikuwa na vitabu vyote tunavyoviita sasa Agano la kale. Hiyo ndiyo Biblia ya Kiyahudi. Lakini wanapoviweka vitabu hivi katika utaratibu  wao na mpanglio,  waliviweka katika makundi matatu.
Kundi la kwanza liliitwa Sheria au Torati, ambapo pia liliitwa vitabu vitano vya Musa. Mwanzo hadi Kumbukumbu la torati.
Kundi la pili liliitwa.Manabii. Kundi hili waliligawanya katika sehemu mbili ambazo ni:
1.     Manabii wa mwanzo     (Yoshua hadi Wafalme)
2.     Manabii wa baadae.    (Isaya hadi Malaki isipokuwa Danieli)
Kundi hili lilihusisha vitabu vya  Yoshua hadi wafalme na Isaya hadi Malaki isipokuwa Danieli.
 Kundi la tatu liliitwa Maandiko.   Ambayo ni Ayubu hadi Mithali na Magombo matano(Wimbo uliobora, Ruth, Maombolezo, Mhubiri, Esta.). Ndipo ilifuatiwa na Danieli, Ezra- Nehemia na Mambo ya nyakati.

Nukuu za Agano jipya zinatoka sehemu zote tatu, 94 kutoka katika vitabu vya sheria, 99 kutoka Manabii na 85 kutoka katika maandiko.

“Tangu damu ya Habili hata damu ya Zekaria….( Luka 11:51 ).

·        Kifo cha Habili,  hii  inawakilisha kitabu cha kwanza katika Biblia   ya kiebrania  ( Mwanzo 4:8 ) Ambacho ni Mwanzo.

·        Kifo cha Zekaria hii huwakilisha kitabu cha mwisho katika Biblia ya kiebrania (Nya 24:20) ambacho ni Mambo ya nyakati.

Hivyo basi Yesu Kristo Bwana wetu alilitambua Agano la Kale lote kama Neno la Mungu.
VI.Muundo wa Agano la  kale katika Biblia yetu.
I. Sheria.                                         
II. Historia.
Iii.Ushairi.
IV. Manabii.

1. Mwanzo
2. Kutoka
3.Mambo ya walawi
4. Hesabu
5. Kummbukumbu la torati.
     Jumla vitabu 5

1. Yoshua
2. Waamuzi
 3 .Ruthu
4 . 1 Samweli
5. 2.Samweli
6. 1Wafalme
7. 2Wafalme wa pili
8. 1 Mambo ya nyakati
9. 2 mambo ya nyakati
10. Ezra
11. Nehemia
12  Esta
Jumla vitabu 12.

1. Ayubu
2. Zaburi
3. Mithali
4. Mhubiri
5. Wimbo uliobora.

1. Isaya
2. Yeremia
3.Maombolezo
4.ezekieli
5. Danieli
6. Hosea
7. Yoeli
8. Amosi
9.Obadia
10. Yona
11. Mika
12.Nahumu
13. Habakuki
14. Sefania
Hagai.
Zekaria
Malaki
 Jumla vitabu 17



Jambo la kukumbuka hapa ni kwamba mpangilio wa vitabu katika Biblia yetu  na ile ya kiebrania ni tofauti na hakuna athali zozote juu ya neno la Mungu kutokana na kutofautiana huko kwa mpangilio.

VII. Sababu za kusoma Agano la Kale.
1. Agano jipya limefichwa ndani ya Agano la Kale.
2. Agano la Kale limefunuliwa ndani ya Agano Jipya.
3. Kile tulichonacho leo ni matokeo ya kile kilichotokea jana.
4. Kile tunachofanya leo kinatengeneza  hali ya kesho.
5. Hatuwezi kulielewa agano jipya bila kujifunza Agano la Kale.
6. Liliandikwa kwaajili yetu pia.

VIII. Nukuu za Agano la Kale katika Agano jipya.
1. Agano jipya lina karibu rejea tofauti 295 toka kwenye Agano la Kale.
2. Imetumiwa mara 224 kwa njia kama “Imeandikwa au Mungu akasema” na ina jumuisha karibu  mistari tofauti 278 kutoka Agano la Kale.
3. Karibu mara 56 waandishi wa Agano la Jipya wanarejea Mungu kama mwanzilishi wa Agano la Kale.
4. Kuna nafsi 41 ambazo kwa njia ya utangulizi iko katika wakati uliopo kama        “ Asema”  sio kama wakati uliopita kama   “alisema”

IX. Tofauti iliyopo kati ya agano la kale na agano jipya.
Kuna tofauti kati ya Agano la Kale na Agano Jipya, tofauti hizo sio zenye kupingana bali ni zenye kujengana, kutegemeana na kuathiliana, hivyo ni tofauti zenye maana.
A. Agano la Kale.
Agano la kale lina sura ya tofauti na Agano jipya katika maeno mbalimbali na tofauti tofauti. Kama ifuatavyo:
1.     Sheria ya nje
2.     Uhusiano na Mungu pekee kupitia kwa kuhani.
3.     Malipo ya dhambi kwa muda
4.     Kumjua Mungu kupitia kwa wale wafundishao.
5.     Utiifu huonesha imani.
6.     Kuhusu watu wote.
7.     Kutokuwezeshwa.
8.     Wakati wa Agano la kale ulimalizika na kifo cha Bwana Yesu.
9.     Umepangwa ili kuonesha mpango wa utakatifu wa Mungu na hali ya dhambi ya mwanadamu.




B. Agano jipya.
1.     Sheria ya ndani.
2.     Uhusiano wa karibu sana na Mungu kibinafsi.
3.     Malipo ya dhambi  milele.
4.     Kumjua Mungu kupitia Roho mtakatifu aishie ndani yetu na Neno la Mungu.
5.     Imani huoneshwa kwa utiifu.
6.     Huhusu mtu mmojammoja.
7.     Ushindi kwa nguvu za Roho mtakatifu.
8.     Wakati wa Agano Jipya ulianza na kifo cha Bwana Yesu pale Msalabani.
9.     Umepangwa ili kuokoa,huonesha utakatifu wa Mungu katika Kristo.


X. Uhusiano uliopo kati ya Agano la Kale na Agano jipya. 
Agano  la kale lina husiana sana na agano jipya kwani vyote vina ujumbe mmoja ambao ni ukumbozi na kiini kimoja ambacho ni Yesu Kristo mwokozi wa ulimwengu. Maagano  hayo yote mawili yanapatana katika mambo yafuatayo.
Agano la kale                                              Agano Jipya.
Huanzisha Ufunuo wa Mungu                          Humalizia ufunuo wa Mungu.
Hutabiri kuwa Yesu ndiye masihi                      Humwonesha Bwana Yesu kuwa    ndiye Masihi.
Huhitaji imani kwaajili ya wokovu                 Huhitaji imani kwaajili ya                            wokovu.
Huhitaji kuishi kwa imani                                Huhitaji kuishi kwa imani.
Hutoa ufahamu kuhusu Mungu na njia zake          Hutoa ufahamu kuhusu Mungu na njia zake
Agano jipya limefichwa ndani ya Agano la Kale    Agano la Kale limefichuliwa                                                         ndani ya     Jipya.
Agano la Kale si kamili  bila Agano jipya     Agano Jipya haliwezi kueleweka bila Agano la   Kale.

Hivyo basi  twaweza kuhitimisha kwa kusema kwamba  Agano la kale si kamili bila ya Agano jipya,hutarajia utimizo wake na kumalizikia katika Agano Jipya.



Zoezi.
Katika makundi ya watu watano watano  jadili maswali yafuatayo.
1.     Nakala za kale zilizogunduliwa kule Kumlani mnamo mwaka 1947 hazina umuhimu wowote katika ukristo na taaluma ya thiolojia kwa ujumla . Jadili kauli hii kwa hoja madhubuti.
2.     Utofauti wa mpangilio wa vitabu katika Biblia ya Kiswahili na kiebrania unadhihirisha dhahili kwamba Biblia yetu imepotoshwa sana. Jadili usemi huu kwa hoja kuntu.
3.     Jadali kauli inayosema kwamba bila  Agano la kale hakuna Agano Jipya.
4.     Eleza umuhimu wa kujifunza Kozi hii ya Pitio la Agsno la Kale.
5.     Si lazima wakristo kusoma na kufuata mafudisho  ya Agano la kale kwa sabbu Agano la Kale ni mahususi kwa wayahudi tu na si watu wote. Pinga kauli hii kwa hoja madhubuti.
6.     Agano la Kale limefafanuliwa ndani ya Agano jipya. Kubali usemib huu kwa hoja madhubuti.


MADA YA PILI:    PENTATUKI.
Malengo ya mada.
Baada ya kumalza mada hii mwanafun zi ataweza:
·        Kueleza maana ya Pentatuki.
·        Kueleza maana ya torati.
·        Kufafanua maana ya kila jina la vitabu vitano vya Musa.
·        Kutaja watu mashuhuri katika kila kitabu
·        Kueleza matukio makuu katika kila kitabu
·        Kutaja mitajo ya Kristo katika kila kitabu
·        Kutaja baadhi ya mafundisho makuu katika kila kitabu
·        Kutaja mistari ya Msingi katika kila kitabu N.k

I. Utangulizi.
Katika mada hii tutatazama vitabu vyote vya Musa kwa muhtasari
Tutachunguza mwandishi, matukio makuu, watu mashuhuri, muundo, mtindo,mafundhisho makuu, mitajo ya Kristo na mistari ya msingi au kiini cha kila kitabu.
Vitabu vitano vya  kwaza vya Biblia hujulikana kama vitabu vya Musa. Pia huitwa Sheria au Torati. Vitabu hivi hufanya katiba ya thiolojia  kwaajili ya taifa la Israeli na pia vina misingi ya kweli iliyodhihirishwa na Mungu  ambapo juu yake ukristo husimama. Vitabu hivi vitano vinatoa taarifa tangu mwanzo wa uumbaji hadi wakati wa matayarisho ya kuingia nchi ya ahadi yaani Kaanani.
Pia vitabu vitano vya kwanza vya Biblia hujulikana kama Pentatuki ambalo ni neno la kiyunani lililotokana na maneno mawili ya kiyunani ambayo ni Penta maana yake tano na Teuchos maana yake kitabu.
Hapo awali vitabu vyote hivi vitano vilikuwa kitabu kimoja tu, lakini viligawanywa kuwa vitabu vitano li kurahishisha kuvitunza katika magombo matano.
Wayahudi walikitaja kitabu cha Pentatuki kuwa sheria tu.(2Nya 17:9,  Neh 8:1-3,18, Mt 5:17,  Luk 24:44).
Kimsingi haiwezekani kuzifahamu vizuri sehemu zingine za Biblia bila ya kuvifahamu vitabu hivi vitano vya kwanza.
Vitabu hivi vitano  ni muhimu sana kwa kwa sababu vinatusaidia  katika kuelewa:
Mungu mwenyewe
Mwanzo wa ulimwengu na mwanadamu.
Msingi wa mawazo ya kithiolojia kama vile
-Dhambi
-Wokovu
-Utakaso
-Imani. N.k.
Mwandishi wa Pentetuki. Katika mapokeo ya Kiebrania na ya Kikristo tangu zamani Musa anatambuliwa kuwa ndiye mwandishi wa Pentatuki.(Neh 8:1, 13:1, Dan 9:11,  Mk 12:26.
Pentatuki yeenyewe  haielezi kwamba Musa ndiye mwandishi wake isipokuwa inaonesha kazi za uandishi ambayo Musa aliifanya. Aliandika sheria ambayo Mungu aliwapa wana wa Israeli Kut 24:4,  34:27,  Kum 31:9,24, Kut 17:14, Hes 33:2. N.k.
Ufunguo katika usomaji wa Agano la kale:
1.     Kuchunguza yale yaliyotokea kwa watu wa Munguwa kale. (Taifa la Israeli na watu wa Agano la kale.)
Matukio yaliyoandikwa katika Agano la kale ni halisi yalitukia kama Agano la kale linavyoeleza.
2.     Kutazama unabii kuhusu Yesu Kristo. Bwana Yesu Kristo ameoneshwa katika kila kitabu cha Agano la Kale. (Mt 5:17-18, Yn 5:39).
3.     Kutazama utimizo binafsi.  Kuangalia kile Agano la Kale linachomaanisha kwetu sasa.



II. KITABU CHA MWANZO.
A.Utangulizi
 Katika vitabu vitano vya Pentatuki kitabu cha kwanza kinaitwa mwanzo. Kitabu hiki kinaelezea kuhusu mianzo ya kila kitu isipokuwa Mungu ambaye hana mwanzo wala mwisho.
Watafsiri wa septuaginta ndio waliotoa jina hili  la “Mwanzo” (Genesis) kwa kitabu cha kwanza cha Biblia kwani Waebrania wa  kale walikiita kutokana na maneno yake ya kwanza yaani “ Hapo Mwanzo”.
Jina la kitabu hili lina asili katika Kiyunani na humaanisha mwanzo wa kila kitu.

B.Kuhusu mwandishi. Kulingana na mapokeo  mwandishi wa kitabu hiki ni Musa. Musa alikuwa mtaalamu wa  kutunga mashairi na Historia. Maisha yake yalikuwa na mahusiano mazuri na Mung.u.(Kum 34:10).

C.Muundo.  Kitabu hiki kina sura hamsini  na migawanyo mikuuu miwili
1.     Mgwanyo wakwanza,  sura ya kwanza hadi ya kumi na moja (1-11).
2.     Mgawanyo wa pili, sura ya kumi na mbili hadi sura ya hamsini.(12-50).
Mpangilio wa visa na matukio ni wa moja kwa moja kwa kiasi kikubwa.

D. Mtindo wa kiuandishi. Kitabu hiki kimetumia mtindo wa  monolojia kwa kiasi kikubwa na daiyolojia  kwa kiasi fulani. Majibizano yanajitokeza wakati wahusika wanajibizana na kutenda katika kitabu.
Mwandishi ametumia Lugha ya kawaida  yenye uwezo wa kueleweka kwa watu wote.Lugha ya kishairi imetumika katika uandishi wa nyimbo na tenzi zinazojitokeza katika kitabu.Mfano sura ya 49.

E. Ujumbe wa kitabu ni Mwanzo wa kia kitu.
F. Mstari wa msingi: Mwanzo 3:15.
Sura kumi na moja za kwanza za  kitabu cha Mwanzo ndio msingi wa Biblia nzima. Katika sura hizo kuna matukio yafuatayo:
1. Uumbaji  (sura ya 1 & 2).
2. Anguko   (sura ya 3).
 3. ahadi ya kwanza ya mwokozi(3:15).
4. Mauaji ya kwanza    (4:1-15).
5. Kuliitia jina la Bwana kwa mara ya kwanza- wana wa Sethi (4:25-26).
6. Mwanzo wa familia  ( 4:1-15).
7. Mwanzo wa ustaarabu wa mwanadamu  (4:16- 22).
8.  Mtu wa kwanza Mwenye imani kuu-Nuhu (6:8-22)
9. Gharika ya kwanza    (sura ya 6-8).
10. Upinde wa mvua Ahadi ya Mungu na ishara ya Agano.  (9:8-17).
11. Mwanzo wa mataifa. (sura ya 10).
12. Kutokea kwa lugha mbalimbali. (11:1-9)
13. Kutawanyika kwa wana wa Nuhu (11:8-32). Wana wa Nuhu walitawanyika na kwenda sehemu zifuatazo:
1.     Uzao wa Yafethi: Walielekea magharibi kuelekea Uhispania  (10:2-5).
2.     Uzao wa Shemu:. Waliishi katika eneo la Kaskazini mwa Ghuba ya Uajemi(10:21:31)
3.     Uzao wa Hamu: Walielekea Kusini mpaka Afrika (10:6-14).

G. Sehemu ya pili
Sehemu ya Pili ya kitabu cha mwanzo ambayo inaanza na sura ya 12 hadi sura ya 50 inazungumzia mwito wa Mungu kwa Ibrahimu na kumfanya taifa kubwa. Mungu alianzisha taifa kupitia Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Yakobo alizaa watoto kumi na mbili wa kiume ambao ndio   waliofanya makabila kumi na mbili ambayo ndiyo taifa la Israeli.
Katika sehemu hii tunajifunza mambo mbalimbali namna Mungu alivyowaita watu na watu walivyoitikia wito huo.

Matuikio hayo ya kitabu cha Mwanzo ndiyo yanayojenga msingi wa mtu kumjua Mungu alivyo na mpango wake mahususi wa kumkomboa mwanadamu kutoka dhambini.
F.  Watu mashuhuri.
1.     Habili
2.     Sethi
3.     Henoko
4.     Nuhu
5.     Ibrahimu
6.     Isaka
7.     Melkizedeki
8.     Nimrodi
9.     Yusufu.N.k,

G. Mitajo ya Kristo.
1.     Isaka.
2.     Melkizedeki
3.     Yusufu.
H. Baadhi ya mafundisho makuu ya kitabu cha Mwanzo.
1.     Mungu ndiye muumba mtawala na mwenye nguvu za kushikilia dunia.
2.     Mungu alimuumba binadamukwa mfano wake wa kiroho  ili awe na ushirika nae.
3.     Mungu alimuumba mwanadamu akiwa  na utashi yaani uhuru wa kuchagua.
4.     Mungu daima ni mwaminifu kwa ahadi zake.
5.     Mungu ana mpango wenye makusudi ya ukombozi ambamo yumo katika
hatua za kuutimiza.
6.     Mungu hupenda wanawe watembee kwa imani.
7.     Tabia ya Mungu haibadiliki.
8.     Mungu huwaacha wanadamu kwa hiari yao wachague kumfuata yeye.
9.     Mapenzi ya Mungu ni kwamba  watu wake wawe na uvumilivu wakisubiri atimize ahadi zake kadri apendavyo yeye na si wao.
10.                        Kutaka kutimiza mpango wa Mungu katka maisha yetu bila yeye Mungu kuhusika ni dalili ya kiburi na kukosa uvumilivu.
11.                        Daima Mungu huamua kumtumia mdogo badala ya mkubwa na  dhaifu badala ya mwenye nguvu.
12.                        Mungu hutazamia ibada toka kwa watu wake.
13.                        Sadaka hugusa moyo wa Mungu.
14.                        Imani huonesha jinsi mtu anavyomjua Mungu.
15.                        Mungu huwatuza watu wanaomheshimu.


III. KUTOKA.
A.Utangulizi
Kitabu cha Kutoka ni kitabu cha pili katika  pentatuki.
Jina la kitabu cha Kutok(Exodus)a lina asili ya kiyunani na maana yake halisi ni kutoka au kuondoka au njia ya kuondoka au njia ya kutoka.
B. Mwandishi. Kulingana na mapokeo mwandishi wa kitabu cha Kutoka ni Musa na inadhaniwa kuwa kitabu hiki kiliandikwa mwaka 1550 au 1500 K.K

C. Muundo. Kitabu kina sura arobaini na kimegawanyika katika sehemu kuu tatu ambazo ni
Sehemu ya kwanza. Utumwa (Sura 1-11).
1.     Waebrania wakiwa nchini Misri.
2.     Taifa kuongezeka
3.     Mwito wa Musa.
4.     Mapigo kumi
5.     Nguvu za Mungu.
Sehemu ya pili.  Ukombozi toka Misri.  (Sura  12-  18).
1.     Malaika wa kifo
2.     Pasaka
3.     Kuondoka Misri
4.     Kuvuka Bahari ya Shamu
5.     Wingu na Nguzo ya moto.
6.     Mana



Sehemu ya tatu. Ufunuo wa Mungu  (Sura  20-40).
1.     Agano la Israeli
2.     Sheria  ya Musa
3.     Sabato
4.     Amri kumi
5.     Maskani Ndama wa dhahabu
6.     Utukufu wa Mungu.

D. Mtindo wa kiuandishi. Kitabu kimeandikwa kwa kutumia mtindo wa monolojia (Masimulizi) na dayolojia kwa kiasi fulani. Pia kitabu kimetumia mtindo wa kiushairi hasa katka nyimbo na Sara  mfano Kut 15:1-21.
Lugha iliyotumika ni rahisi na yenye kueleweka kwa wasomaji wote . Kitabu hakina tamathali za semi zenye kiwango cha kumchanganya msomaji

E.Ujumbe  wa kitabu . Mungu ni  Mkombozi.      Musa aliandika katika kitabu hiki cha Kutoka  ukombozi wa ajabu wa Mungu kwa watu wake, Israeli kutoka katika kifungo cha utumwa na dhambi na ufunuo wake yeye mwenyewe na uadilifu wake kwao ili awaoneshe kwamba Mungu ndiye Mwokozi na mkombozi.


Katikati  ya mwazo na kutoka  Familia ya Mungu ilikua kwa kasi  na kuwawa ni taifa kubwa . Wana wa Israeli waliingia Misri wakiwa watu 70 yaani mzee Yakobo, watoto wake, wake za watoto wake na watoto wao, jumla yao wakiwa sabini.
Baada ya miaka mianne  (400)  familia hii ya watu sabini ilikuwa na kuongezeka kwa kasi sana na kufikia  karibu milioni tatu na kuwa taifa kubwa na hodari.

Tukio muhimu sana katika Agano la kale limeorodheshwa katika sura ya kumi na mbili mpaka kumi na nne. Sura hii inahusu ukombozi wa kila mwisraeli kupitia damu ya mwanakondoo wa pasaka na nguvu ya Mungu walipovuka bahari ya shamu.
Tukio la kutoka kwa wana wa Israeli Misri ni muhimu sana na linatazamwa kama kivuli cha  waamini wote kuokolewa kutoka katika utumwa wa dhambi na nguvu ya dhambi.
Waisraeli waliokolewa kwa damu ya mwanakondo wa pasaka sisi tunaokolewa kwa damu ya mwanakondoo wa Mungu Yesu Kristo. Yn 1:29.
 Katika kitabu hiki kuna taashira mbalimbali au mitajo mbalimbali inayosimama badala ya kitu kingine.Baadhi ya taashira hizo ni:
1.     Musa anamwakilisha Bwana Yesu Kristo.
2.     Farao  anamwakilisha shetani
3.     Misri inawakilisha ulimwengu wa dhambi.
4.     Wana wa Israeli watu walio dhambini wanaohitaji kuokolewa.

F. Mitajo ya Kristo.
1.     Musa. Mkomobzi
2.     Haruni- Kuhani mkuu
3.     Mwanakondoo wa pasaka.
4.     Damu ya mwanakondoo wa pasaka.
5.     Mana

G. Matukio Makuu.
6.     Mateso katika nchi ya ugeni
7.     Mauaji ya Musa
8.     Wito wa Musa
9.     Mapigo kumi ya wamisri
10.            Kuondoka Misri
11.            Kuvuka bahari ya Shamu
12.            Muujiza wa Maana jangwani
13.            Kutolewa kwa sheria katika mlima Sinai
14.            Ndama wa dhahabu.
15.            Maagizo ya ya ujenzi wa  Hema ya kukutania.
16.            Agano la Mungu na Isareli kupitia mtumishi wake Musa.

F.  Watu mashuhuri.
1.     Farao
2.     Musa
3.     Haruni
4.     Miriamu
5.     Yethro

G.Mapigo Kumi Ya Wamisri.
1.     Pigo laMaji kuwa damu.
2.     Pigo la Vyura.
3.     Pigo la Chawa
4.     Pigo la Nzi
5.     Pigo la majipu.
6.     Pigo la Tauni
7.     Pigo la Mua ya mawe
8.     Pigo la Nzige
9.     Pigo la Giza
10.                        Pigo kuu lakifo cha mzaliwa wa kwanza wa kila kitu katika jami ya wamisri..
Jambo la msingi na kukumbuka hapa ni kwamba Mungu aliwalinda watu wake Israeli. Mapigo yote haya yaliwapata wamisri lakini wana wa Israeli walikaa salama katika  Eneo la Gosheni walililopewa na Farao kuwa makazi yao .Halikuwapata pigo lolote kwani Bwanaa alikuwa upande wao.

H. Mafundisho makuu ya kitabu. Yafuatayo ni baadhi ya mafundisho makuu yanayopatikana katika kitabu hiki cha Kutoka:
Mungu pekee ndiye anaestahilikuabudiwa
1.     Mungu ni mwaminifu kwa ahadi zake
2.     Mungu anapomwita mtu kwaajili ya huduma humpa upako wa kumwezesha kufanya huduma hiyo.
3.     Hakuna sababbu zinazokubalika kukataa mwito wa Mungu.
4.     Mungu huchukua jukumu la kuwaumba watu vile walivyo kwaajili ya utukufu wake.
5.     Ibada hukamilika kwa dhabihu.
6.     Ibada hufanya kwa maelekezo ya Mungu mwenyewe.
7.     Uwezo wa Mungu ni mkuu kabisa kuliko ule wa miungu.
8.     Mungu huheshimu mgawanyo wa majukumu na utoaji wa mamlaka kwa wale watu wawezao, wacha Mungu na waaminifu.
9.     Mungu anahitaji watu wawe na masuhiano safi na yeye na wao kwa wao
10.                        Sheria za Mungu ni takatifu na zilitolewa ili zifuatwe.
11.                        Mungu hupenda kukaa miongoni mwa watu wake na kushirikiana nao.



IV. MAMBO YA WALAWI.
A. Utangulizi.
Jina la kitabu hiki liatokana na neno la kilatini “Leviticus”. Lenye maana ya walawi.Mambo ya kitabu hiki ni ya wakati wana wa Israeli wakiwa chini ya mlima Sinai wakiwa safarini kueleka nchi ya ahadi.Kufuatana na ahadi yake Mungu kwa Ibrahimu aliwatoa waisraeli kutoka utumwani Misri na kuwaweka  katika njia                        kuelekea Kaanani. Baada ya miezi mitatu walifika katika mlima Sinai au Horebu, mahali walipokaa karibu mwaka mzima. Katika muda ule walijiandaa kwa maisha mapya yaliyokuwa yanawakabili.Kut 19:1, Hes 10:11.

Kabla ya kuelekea katika nchi ya ahadi Mungu aliwaelekeza Waisraeli  kwa kirefu sana  Jinsi walivyotakiwa kumwabudu yeye na kufuata utaratibu wa matoleo yaliyo ambatana na dhabihu za wanyama kwenye maskani ya ibada.
Mungu alitaka watu wake wawe watakatifu kama yeye alivyo mtakatifu. Law 15:13, !8:1-5.
Katika sura ya kwanza hadi ya tano Mungu alitoa aina tano za matoleo. Aina tatu za  kwanza zilikuwa za hiari na ziliwekwa ili kuhakikisha kujitoa binafsi na kujiweka mikononi mwa Mungu.
Sadaka za aina mbili za mwisho zilikuwa za dhambi, hatia na msamaha wa dhambi. Hizi zilikuwa ni sadaka za lazima na ziliitwa sadaka za dhambi na  hatia. Sadaka za aina hii zilihusika na kuleta msamaha wa dhambi, mtu alizotenda.
Katika sura ya kumi vifo vya wana wawili wa Haruni Nadabu na Abihu vilionesha jinsi Mungu asivyo na mchezo kuhusu mtu kuwa mtakatifu.

B. Kuhusu mwandishi wa kitabu. Kwa mujibu wa mapokeo mwandishi wa Kitabu cha Mambo ya walawi ni Musa.Inadhaniwa kuwa imeandikwa katikati ya miaka ya 1550 na 1530. K.K
C. Muundo wa kitabu. Kitabu cha Mambo ya Walawi kina sura ishirini na saba (27) na kimegawanyika katika sehemu kuu mbili ambazo ni.

1. Sehmu ya kwanza. Dhabihu(sura 1-10).
·        Kumwabudu Mungu.
·        Matoleo matano ya dhabihu.
·        Dhabihu za wanyama
·        Ukuhani wa Haruni

2. Sehemu ya pili:Utakaso (sura 11-27)
Kutembea na Mungu.
·        Sheria za usafi na unajisi.
·        Siku ya upatanisho.
·        Dhabihu za damu
·        Maisha ya utakatifu
·        Sikukuu saba za Israeli.

D.Mtinbdo wa kiuandishi.Mwandishi ametumia mtindo wa monolojia tangu mwanzo hadi mwisho wa kitabu.
Lugha iliyotumika ni ya kawaida yenye kueleweka karibu  na wasomaji wote wa kawaida
.
E.Msitari wa msingi ni  Law 17:11.

D. Ujumbe wa kitabu:  ni Utakatifu.

E. Ufafanuzi wa sadaka mbalimbali.
1. Sadaka za kuteketezwa
Sadaka hii ilikuwa ni kwa kila mtu kwani ilikuwa ni kwaajili ya kufunika dhambi. ya mtu mmoja mmoja.
Alitolewa mnyama asiye na kasoro yoyote.(mfano kondoo, ng’ombe au njiwa kulingana na uwezo wa mtu).


2. Sadaka ya chakula.
Walitoa unga au nafaka.
Sadaka hii iliwakilisha shukrani kwa Mungu na kujiweka wakfu kwake.

3.Sadaka ya amani.
Hii ilikuwa ni sadaka ya hiari iliyokuwa inaonesha upendo wao kwa Mungu.
Mnyama asiye na kasoro alitumika katika ibada hii.
Sehemu chache kadhaa za nyanma mtoaji alichukua ili kufurahia cha kula chake  na marafiki zake kama ishara ya ushirika na  walipaswakula mbele za Bwana.


4. Sadaka ya dhambi.
Hii ilihusika na utakaso wa eneo fulani lililohusika. Mtoaji alihusika kama vile kuitakasa hema ya kukutania na madhabahu yake.(Law 9:8-11).
 Ilikuwa sehemu ya malipizi iliyokuwa ikifanywa mara moja kila mwaka.(16:11-14).

Sadaka ya hatia.
Ilihusika kuleta utakaso kwa mtu binafsi kama amechukua kitu ambcho kilikuwa ni mali ya Mungu, au mali ya mwingine. Mfano fungu la kumi au kitu cha ndugu yake. Sheria iliagiza mtu alete kondoo dume asiye na kasoro yoyote.

Jambo la kukumbuka na kuzingatia hapa ni kwamba sadaka zote hapo juu zilimwakilisha Yesu na Huduma yake kama Kuhani mkuu wetu.
Sadaka hizo zinaelezea pia utakatifu wa Mungu wetu na kutudai kuwa na mwenendo wa kiuadilifu.(Ebr 6)
F. Watu mashuhuri.
1.     Musa
2.     Haruni(Kuhani mkuu)
3.     Makuhani
4.     Walawi.
G. Mafundisho makuu.
1.     Mungu ni mtkatifu hivyo anadai watu wake kuwa watakatifu kama yeye.
2.     Utakatifu huhusisha usafi, kujitenga na kuwa tofauti kabisa.
3.     Msamaha wa dhambi hupatikana kwa njia ya dhabihu ya kafara mbadala.
4.     Dhaibu hutolewa kwa kadri ya maelekezo ya Mungu mwenyewe.
5.     Utakatifu ni mwenendo wa maisha ya kila siku.
H. Mitajo ya Kristo.
Katika kitabu hiki cha kutoka sadaka zote zinazotajwa ni kiwakilishi cha Yesu Kristo. N.k

Tunaweza kuhitimisha kwa kusema kwamba kitabu cha Mambo ya walawi ni katiba ya ibada ya Wana wa Israeli. Mungu aliwapa mwongozo wa namna wanavyopaswa kuishi katika nchi ya ahadi alikokuwa anawapeleka. Aliwapa sheria, kanuni na taratibu. Jumla ya sheria zote zilikuwa 613 ambazo Mungu aliwapa wana wa Isreli. Zikiwa zimegawanyika katika makundi kadhaa. Mfano sheria za kiraia, sheria za kidini n.k. sheria zote hizo zinapatikana katika pentatuki yote.


V.  HESABU.
A. Utangulizi
Kitabu hiki cha Hesabu ni kitabu cha nne katika pentatuki. Jina la kitabu hiki linatokana na sensa ambayo Musa aliifanya kabla ya kuondoka katika mlima Sinai. Biblia ya kiebrania inatumia jina la jangwani na kwa kweli jina hili lina sadifu yale yaliyomo ndani ya kitabu kwa sababu kitabu hiki kinaelezea habari ya safari ya waisraeli toka mlima Sinai hadi mpakani mwa nchi ya Kaanani. Na sehemu kubwa ya safari hiyo ilikuwa ni jangwani.
B. Kuhusu mwandishi wa kitabu. Kwa mujibu wa mapokeo kitabu hiki kiliandikwa na Musa.Tarehe yake ya kuandikwa  haitofautiani na ile ya Warawi na kutoka.

C. Muundo wa kitabu. Kitabu hiki kina sura therathini na sita(36) na kinagawanyika katika sehemu kuu tatu ambazo ni:
Sehemu ya kwanza.Maagizo(sura 1-10)
Sehemu ya pili. Kujaribiwa  (sura 11-21)

Sehemu ya tatu.Maagizo.(sura 22-36)
D. Mtindo wa kiuandishi. Kitabu hiki kimetumia mitndo wa Monolojia kwa kiasi kikubwa na daiolojia kwa kiasi kidogo. Pia kimetumia lugha ya kishairi hususani katika sura ya 21 hadi 24.
Lugha iliyotumika ni nyepesi yenye kueleweka karibuni na wasomaji wote wa kawaida.

E. Ujumbe wa kitabu. Kutangatanga jangwani.
Mungu hutaka watu wake watembee kwa imani na wanaposhinwa kufanya hivyo  Hukosa Baraka muhimu za Mungu na kusababisha Mungu awaadhibu.

F.  Mstari wa msingi          Hes 14:20-24.

G. Matukio muhimu.
1.     Safari ya wana wa Israeli toka Sinai hadi kadeshi miaka miwili.
2.     Kuzunguka Kadeshi Barnea  miaka therathini na nane.
3.     Wapelelezi kumi na wawili kupeleleza nchi ya ahadi.
4.     Kuadhimishwa kwa pasaka ya kwanza.
5.     Nyoka wa moto na nyoka wa shaba.
6.     Sensa ya wana wa Israeli.
7.     Kifo cha Haruni.
8.     Kifo cha Koran na wenzake.
H.  Watu mashuhuri.
1.     Musa
2.     Haruni.
3.     Miriamu
4.     Yoshua
5.     Karebu
6.     Kora
7.     Finehasi
8.     Eleazari
9.     Baalamu.

I.  Baadhi ya mafundisho makuu.
1.     Mungu anatarajia moyo wa utIi na shukrani toka kwa watu wake.
2.     Mungu anahitaji watu wake wawe wavumilivu.
3.     Mungu anataka watu wake waishi kwa imani
4.     Mungu anataka watu wake waheshimu mamlaka aliyoiweka.
5.     Dhambi huleta madhara katika roho na katika mwili.
6.     Kunung’unika ni hatari sana.
7.     Kutokuwa na imani ni dhambi.
8.     Tunaposhindwa kumwamini Mungu hupelekea kukosa  Baraka zake.
9.     Mgwanyo wa majukumu ni muhimu sana ili kuweza kuleta ufanisi katika uongozi.
10.                        Mungu ni mwaminifu kwa ahadi zake zote yaani katika kubariki na katika kuadhibu.


J. Mitajo ya Kristo.
1.     Nyoka wa shaba.
2.     Mwamba uliotoa maji.
3.     Mana.
4.     Miji ya makimbilio
5.     Nguzo ya wingu na ya moto.
Jambo la kukumbuka hapa ni kwamba kitabu hik cha Hesabu kinaelezea safari ya wana wa Israeli toka mlima Sinai paka mpakani mwa nchi ya Kaanani. Ni kitabu cha safari. Kinaeleza changamoto mbalimbali walizokutana nazo wana wa Israeli katika safari yao na namna walivyoitikia changamoto hizo na matokeo yake.
Kitabu hiki kinatoa picha ya safari yetu ya kwenda Mbinguni kwamba kuna changamoto mbalimbali ambazo tutakutana nazo. Namna tunavyoitikia changamoto hizo itaamua  na kuathili safari yetu. Hivyo ni lazima kuwa wavumilivu na wanyenyekevu. Kwa sababu Mungu ni Mwaminifu kwa ahadi zake atatimiza kila kitu alichokisema kwa wakati wake. Tusiwe wepesi kukata tamaa, kulalamika na kunung’unika kwani hii huonesha kukosa imani na kusababisha tushindwe kupata baraka  alizotuandalia Mungu wetu.Tutembe kwa imani na kwa ushujaa mkuu.


V.KUMBUKUMBU LA TORATI.
A. utangulizi
Jina la kitabu hiki linatokana na neno la kiyunani “Deuteronomium” lenye maana ya sheria ya mara ya pili. Jina hili lilitolewa na watafsiri 70 waliotafsiri Biblia kwa mara ya kwanza katika lugha ya  Kiyunani. Jina hilo linatokana n muungano wa maneno mawili ambayo ni deuteros likimaanisha pili na nomos likimaanisha sheria.
Katika kitabu hiki Musa anakifundisha kizazi kipya hatima ya kumiliki nchi ya ahadi na njia mpya ya kuishi.
Kitabu hiki kiliandikwa katika uwanda wa Moabu, wana wa Israeli walipokuwa karibu kuvuka mto Yordani na kuingia  kuimiliki nchi ya ahadi.
Mua aliwaonya kuhusu hatari ya kurudia makosa kama walivyofanya baba zao hapo awali.
Kwa hiyo tene na tena Musa alisema “ Kumbuka”  kuwu waangalifu, msisahau, sikilizeni kwa umakini. Msirudie makosa tena kama walivyotenda baba zenu.1Kor 10:1-11.
Taifa hili lilikuwa limefika mahali palepale walipokuwa wamefika miaka 38 iliyopita. Wakati huu sasa wanapaswa kumtii Mungu na kuwa waaminifu kwake ili waingie katika nchi ya ahadi.
Mungu alikuwa anataka kuwaingiza wana wa Israeli katika nchi ya ahadi, wao walichokuwa wanapaswa ni kuwa waaminifu na watiifu kwake.
Katika kitabu hiki Musa anarudia  kufundisha kwa upya sheria ya Mungu kwa kuwa kizazi hiki si kile cha wakongwe kilichotoka Misri bali ni watoto wao ambao walipaswa kukumbushwa  yale ambayo Mungu alisema na baba zao. Ndiyo maana inaitwa sheria ya mara ya pili.

B.  Kuhusu mwandishi.Kulingana na mapokeo mwandishi wa kitabu hiki ni Musa. Inadhainwa kuwa sura ya mwisho ya kitabu hiki iliandikwa na Yoshua.

C.Muundo wa kitabu. Kitabu hiki kina sura therathini na nne(34) na chaweza kugawanywa katika sehemu tatu ambazo ni kama hotuba, Musa akihutubia kizazi kipya. Sehmu hizo ni :
Sehmu ya kwanza.  Kutazama nyuma.(Historia ya Israeli) sura ya kwanza mpkaa ya tatu.(1-3)

Sehemu ya pili. Kutazama ndani. (sura ya nne hadi sura ya ishirini na sita ,4-26). Kulitambua Agano la Mungu wao. Wao ni taifa teule  kwa hiyo wanapaswa kutii sheria ya Mungu wao.

Sehemu ya tatu . Kutazama mbele.(Maandalizi ya safari)  sura ya ishirini na saba hadi therathini na nne. (27-34). Maagizo ya mambo ambayo walipaswa kufanya baada ya kuingia katika nchi ya ahadi.

D.Lengo la Mungu.
Alitutoa nje ili atuingize ndani
Wokovu si mwisho bali ni mwanzo wa maisha mapya.
E. Hatari ya mafanikio.
Musa aliwaonya kuhusu mafanikio aliwaambia kwamba waangalie sana kwa sababu mafanikio yaweza:
1.     Kuwafanya wamsahau Mungu wao.
2.     Kuwapa majivuno kwamba ni kwa nguvu zao wenyewe wamefanikiwa.
F. Laana na Baraka.
Musa aliwaeleza na kuwafundisha umuhimu wa kulitunza Agano la Mungu  na Baraka zilizoambatana na laana iliyoambatana kutokana na kulivunja Agano la Mungu.
1.     Tabia ambazo hazipendezwi na Mungu Kum 27:14-26.
2.     Baraka kwa utii    Kum 28.1-14.
3.     Laana kwa kutotii a uasi Kum 28:15-48.


G.Agano la nchi ya ahadi. Kum 29:10-14.
Ahadi ya kutunza Agano ni kubaki katika nchi ya ahadi na alama ya agano itakuwa ni kuwahi au kuchelewa kwa mvua  Kum 11:13-14.

H.Maagizo kwa Yoshua. Kum 31:6-8.

I. Kubarikiwa kwa makabira kumi na mbili ya wana wa  Israeli (Sura 32-33).

J.Kifo cha Musa na Yoshua kuchukua uongozi.  Kum 34:5-9.

K. Baadhi ya mafundisho makuu ya kitabu.
1.     Mungu hutaka utii kamili.
2.     Kila itikio la mwanadamu  ju ya agano la Mungu lina matokeo yake
3.     Mungu hututaka sisi kuwafundisha watu wengine Neno lake kwa  usahihi.
4.     Ni raishi kumsahau Mungu wakati wa Mafanikio.
5.     Mungu anaheshimu uchaguzi wa mtu.
6.     Amri za Mungu ni kamilifu kabisa.

L.Watu mashuhuri.
1.     Musa
2.     Yoshua.
3.     Makuhani.

M. Mitajo ya Kristo.
·        Musa.
·        Yoshua.
N. Matukio muhimu.
 Matukio muhimu katika kitabu hiki ni  kurudiwa kwa mafunzo ya sheria kwa kizazi kipya cha wana wa Israeli na kifo cha Musa mtumishi wa Bwana.
                                                  


Zoezi.
Katika makundi ya watu watano watano jadili maswali yafuatayo.
1. Taja majina ya watoto kumi na mbili wa Yakobo wapange kulinana na mama zao.
2.Chora mti wa familia tangu Adam hadi makabila kumi na mbili ya Israeli.
3. Chora mti wa ukoo/familia  ukionesha orodha ya vizazi tang Ibrahimu hadi taifa la Israeli.
4. Changanua family ya  Yakobo iliyoingia Misri kwa kutaja uzao wa kila mtoto.
5. Jadili mwanzo wa ustaarabu duniani na athali zake.
6. Toa sababu za Farao kuanza kuwatesa wana wa Israeli.
7. Jadili sababu za Mungu kuufanya moyo wa Farao kuwa mgumu.
8. Jadili athali za kutii nusunusu  mwito wa Mungu.
9.Jadili umuhimu wa kujifunza Pitio la Agano la kale.
10. Jadili mapigo kumi Mungu aliyowapiga wamisri.
11. Vitabu vitano vya  Musa asili  yake ni kitabu kimoja kilichoitwa Pentatuki. Jadili kauli hii.
12.Jadili mambo ambayo wana wa Israeli waliagizwa kuyafanya mara tu baada ya kuingia nchi ya ahadi .
13. Changanua vipimo na vitu mbalimbali vilivyohitajika katika ujenzi wa hema ya kukutania (maskani)kule jangwani.
14. Eleza sababu za msingi za kugawanya kitabu kimoja na kutokea kwa vitabu vitano vya Musa badala yakuwa  kitabu kimoja.

No comments:

Post a Comment