Tena
ufalme wa Mbinguni umefanana na hazina
iliyositirika katika shamba ambayo mtu alipoiona aliificha; na kwa furaha
yake akaenda akauza alivyokuwa navyo vyote, akalinunua shamba lile.
Ndugu mtu wa Mungu napenda kukuletea tena somo hili linalohusu
hazina iliyositirika. Hazina ni kitu cha thamani ambacho hakipatikani kwa
urahisi. Kitu hiki kinapopatikana huleta
mabadiliko makubwa kwa aliyekipata.
Tazama mfano uliotolewa na Bwana
wetu Yesu Kristo hapo juu “Ndani ya
shamba kulikuwa na hazina ambayo
ilivumbuliwa na mtu mmoja, mara
baada ya kuivumbua alikwenda akauza kila kitu alichokuwa nacho na kisha kulinunua lile shamba.
Hazina ni kitu muhimu sana. Kila
mwanadamu alieumbwa na Mungu ndani yake kuna hazina zirizositirika. Ni wajibu
wa kila mtu hasa mtoto wa Mungu
kuvumbua hazina zilizo ndani yake na
kuzifanyia kazi na hapo ndipo kusudi la maisha linapokuwa limefikiwa.
Zinahitajika jitihada za makusudi na
kukubali kujitoa dhabihu, kuwa tayari kupoteza kila kitu ili kusababisha kuzaliwa na kile Mungu ameweka ndani yako.
Tazama mfano wa Ngano alioutoa Bwana
wetu Ysu Kristo katika Injili ya Yohana 12:24
Amini, amini, nawaambia, chembe ya ngano isipoanguka katika nchi,
ikafa, hukaa katika hali hiyo hiyo peke yake; bali ikifa hutoa mazao
mengi.
Kumbuka Yesu Alisema ngano Isipokufa
hubaki katika hali hiyohiyo, ni lazima
ngano ife ili iweze kumea na kuleta mazao mengi, katika kanuni ya uzazi wa mimea tunajifunza kuwa
ndani ya kifo hutoka maongezeko na mazidisho. Ni lazima ukubali
kufa katika kutimiza kile Mungu ameweka
ndani yako. Hupaswi kujihurumia hakuna
mafanikio yasiyo na maumivu. Kubali kulipa gharama katika kuvumbua kile Mungu
ameweka ndani yano na uweze kusababisha
kitokee kabla hujaondoka duniani.
Hebu pitia somo hili
ukiwa katika hali ya maombi, Mungu atakufunulia kweli yake takatifu
kupitia somo hili. Nakuhakikishia kuwa utakapoamua kufanyia kazi kweli Mungu
alizokufundisha kupitia somo hili kamwe
htabaki vile ulivyo. Maisha yako na huduma yako itabadilika na kuwa
katika viwango ulvyokusudiwa na Mungu.
Karibu tujifunze pamoja.
Myles
Munroe ambaye ni kiongozi Mkristo alisema hivi kuhusu uwezo wa mwamini kufanya
kitu katika kitabu chake kiitwacho Understanding Your Potential:
“Mahali penye utajiri sana hapa duniani si
katika maeneo ya mafuta huko Kuwaiti, Iraki au Saudi Arabia. Wala si katika
machimbo ya dhahabu na almasi huko Afrika Kusini, au machimbo ya uranium huko
Urusi au katika machimbo ya shaba yaliyoko Barani Afrika. Utashangaa tu lakini,
utajiri mkubwa sana katika dunia yetu uko mita chache tu kutoka nyumbani kwako.
Uko katika makaburi yenu. Huko chini, kumezikwa ndoto ambazo hazikuwahi
kutimizwa, nyimbo ambazo hazikuwahi kuimbwa, vitabu ambavyo havikuandikwa,
picha ambazo hazikuchorwa, mawazo ambayo hayakutolewa, maono ambayo
hayakufanyika uhalisi, vitu vilivyobuniwa ambavyo havikutengenezwa, mipango
ambayo haikutoka kwenye mawazo ya mtu na makusudi ambayo hayakutimizwa. Makaburi
yetu yamejaa uwezo wa kufanya vitu ambao haukufanikiwa.
“Uwezo wa kufanya vitu unadai kwamba usikubali
kutosheka na kitu ulichofanikisha. Adui
mmoja ambaye ni mkubwa sana wa uwezo wako kufanya vitu ni mafanikio.
Mafanikio kidogo huharibu uwezekano mkubwa! Ili uweze kufikia uwezo wako kamili
wa kufanya vitu, hutakiwi kutosheka na ulichofanikisha. Pia ni muhimu kwamba
usiruhusu kile usichoweza kufanya kiingiliane na kile unachoweza kufanya.
Janga
kuu maishani si kifo, bali ni maisha ambayo hayakufikia kilele chake katika
uwezo wa kufanya vitu.
Katika kurahisisha dhana hii, hebu tutazame kitu
kimoja katika uumbaji ambacho kina nguvu sana kitu hicho ni mbegu.
Nikishika
mbegu mkononi na kuukuliza, ‘Nina nini mkononi?’ utasemaje? Pengine utajibu
kilicho wazi kabisa una mbegu. Lakini, ukielewa asili ya mbegu, jibu
lako linaweza kuwa uhalisi japo halitakuwa ukweli. Ukweli ni
kwamba nimeshika msitu mkononi mwangu.
Ni hivi: Katika kila mbegu kuna mti, na katika kila mti kuna matunda au maua
yenye mbegu ndani yake. Na hizo mbegu nazo zina miti ambayo ina matunda yenye
mbegu ndani yake ambazo
zina miti yenye matunda yenye mbegu, na kadhalika na kuendelea.
Unachokiona hapa si yote. Kwa hiyo, tofauti kati ya
mbegu moja na utoaji wa chakula kama vile ngano inayoweza kulisha dunia nzima
ni kitu kinachoitwa ‘uwezo wa kufanya
vitu.’ Hicho ndicho kiwango cha tofauti kati ya unachoona na
kinachowezekana
Kama Musa angekufa kabla
hajaona kile kichaka kilichokuwa kinawaka moto au Paulo kabla ya kukutana na
Yesu akiwa njiani kwenda Dameski au
Ibrahimu kabla ya Isaka kuzaliwa. Maandiko na historia vingekuwa tofauti sana.
Kama Martin Luther angekufa bila ya kuandika zile hoja zake (Thesis) au Charles Wesley bila
ya kutunga nyimbo zake au John Wycliff bila kufasiri Biblia katika
lugha ya Kiingereza. Historia ya Kanisa ingekuwa tofauti sana.
“Sijui
ingekuwaje kama baba yako angekufa kabla hujatungwa mimba, au mama yako kabla
hujazaliwa. Dunia ingepoteza nini kama usingezaliwa? Je, dunia itakosa nini kwa
sababu unashindwa kuishi kufikia kiwango cha uwezo wako wote? Je, utakwenda
kaburini na nyimbo, vitabu, magunduzi au dawa?”
Je, inawezekana
kwamba dhambi kuu ya Wakristo imo katika uwezo wao wa kufanya mambo ambao
haujafikiwa? Tena, uwezo mkuu wa kufanya mambo ambao haujatumiwa katika siku za
leo ni katika eneo la kutimizwa Agizo Kuu la Bwana wetu. Yeye amekupa wewe nafasi maalum katika Kuufikia
Ulimwengu Kikamilifu, na ni nafasi
kubwa kuliko yoyote uliyowahi kuwa nayo. Hii nafasi haiwezekani bila ya maono
kwamba inawezekana.
Basi, kitu muhimu
kuliko vyote katika maisha yako ni kuwa na maono yanayokubaliana na Mungu, na
kuyafuatilia. Kwa kuwa kazi uliyopewa inahusu dunia nzima, maono
yako lazima yawe hivyo hivyo. Je, una maono ya aina hiyo?
Sasa – watu kama wewe na mimi – wenye ubinafsi, kujijali,
wenye kujali kwao na wenye kujiona wanapataje maono ya Mungu? Angalia kanuni
hii, inayoweza kufanya kazi: habari sahihi ukijumlisha na kuangaziwa
kiroho vitaleta maono, ambayo yatasababisha motisha, na hiyo
motisha itapelekea utendaji wa kiroho wenye matokeo. Hapo, ona kwamba
maono huanza kwa kupata habari sahihi. Sawa na ambavyo kuona kimwili
kunavyoanza kwa kuwepo kwa kivutio cha nje, ndivyo na maono kiroho yanavyoanza
kwa ukweli wa Mungu katika Maandiko na kila kitu ambacho kinahusiana na
Maandiko.
“Matofali” ya
kujengea maono hayo ni: kufahamu Maandiko kiasi cha kutosha na moyo sikivu wa
kusikia sauti ya Mungu na kuitii, halafu
ufahamu wa jiografia ya dunia na tamaduni za nchi mbalimbali, utambuzi kiroho
wa matukio, maombi, kujisomea ili kupata habari, ujuzi binafsi (“njoo uone”
katika Maandiko) baadhi ya maeneo ya kimisheni duniani,
ushirikiano na waamini wenye maono, kujitoa
kwa ajili ya kutoa kuhusu mambo ya umisheni, kukutana na wamishenari na
Wakristo wenye kugusa dunia, na maamuzi mbalimbali katika maisha. Unaweza
kuanza kushirikiana na Mungu katika kujenga maono ya kiroho katika maisha yako
leo. Lakini, ni dhahiri – na inasikitisha sana – kwamba Wakristo wengi
unaoshirikiana nao mara kwa mara hawana maono kama hayo.
Omba Mungu
akupe kutambua kusudi la kuumbwa kwako kwa sababu hakuna mwanadamu
aliyekuja kwa bahati mbaya katika dunia hii. Mungu anakusudi la kipekee na kila
mtu.
Ninaamini kwamba ikiwa kila mtu angetimiza walau hata kidogo kusudi lake la kuwepo hapa duniani, dunia hii
ingekuwa ya tofauti sana. Watu wengi wanaishi nje ya makusudi yao ya kuwepo hapa duniani. Soma
Neno la Mungu na jenga utaratibu wa
kuketi barazani pa Mungu ili
akusikizishe ili uweze kutambua kusudi lako la kuwepo hapa duniani na kutambua
laslimali ambazo Mungu ameweka ndani yako na
namna unavyowea kutenda katika kutimiza kusudi lako. Kila mtu ni wa
kipekee na ndani yake kuna vitu vya kipekee vinavyomfanya awe wa kipekee.
Tatizo kubwa
katika dunia ya sasa ni Maigizo.
Watu wamekuwa wavivu wa kugundua
hazina ambazo Mungu amaweka ndani yao na wamekuwa wakiiga vitu kutoka
kwa watu wengine wanaodhani kuwa ni maarufu. Watu wamekuwa waigaji. Wahubiri
wanaiga wahubiri wenzao, waimbaji wanaiga waimbaji wenzao nah ii imeleta
ukasuku katika huduma na katika maisha
ya kawaida. Kuiga si kubaya na ila kunapochukua nafasi na kusababisha mtu ashindwe kujifunza na
kuvumbua hazina iliyoko ndani yake hap ndipo
kuiga kunapokuwa tatizo.
Tafuta kujua ni hazina zipi Mungu ameweka ndani yako
na namna gani unaweza kuzifanya zikatokea, wawweza kuvumbua kwa njia
zifuatazo:- Soma Neno la Mungu, Soma
Vitabu mbalimbali vilivyoandikwa na
watumishi wa Mungu na kisha kuwa na ushirika
wa kudumu na Mungu kwa njia ya Maombi, kuwa karibu na watumishi wa Mungu kwaajili ya malezi yaani uwe na baba wa
kiroho kwaajili ya malezi na maongozi.
Ni maombi yangu kwa Mungu kwamba usife bila kutimiza kusudi mahususi la
kuumbwa kwako. Usife bila kutoa mchango wako ambao Mungu ameuweka ndani yako.
Dunia hii bado inasubiri mchango wako kwani ni wa muhimu sana.
Kwa mafundisho zaidi piga simu Simu no. 0762532121/0765992774
Wako katika Mavuno ya Kiroho
_________________
Rev.Dr. Erick L Mponzi
MKURUGENZI MKUU
ELAM CHRISTIAN HARVEST
SEMINARY