Tuesday, 26 December 2017

HAZINA ILIYOSITIRIKA



Tena ufalme wa Mbinguni umefanana na  hazina iliyositirika  katika shamba  ambayo mtu alipoiona aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyokuwa navyo vyote, akalinunua shamba lile.
    Ndugu mtu wa Mungu  napenda kukuletea tena somo hili linalohusu hazina iliyositirika. Hazina ni kitu cha thamani ambacho hakipatikani kwa urahisi. Kitu hiki  kinapopatikana huleta mabadiliko makubwa kwa aliyekipata.

Tazama mfano uliotolewa na Bwana wetu Yesu Kristo hapo juu  “Ndani ya shamba kulikuwa na hazina ambayo  ilivumbuliwa na mtu  mmoja, mara baada ya kuivumbua alikwenda akauza kila kitu alichokuwa nacho  na kisha kulinunua lile shamba.

Hazina ni kitu muhimu sana. Kila mwanadamu alieumbwa na Mungu ndani yake kuna hazina zirizositirika. Ni wajibu wa kila mtu  hasa mtoto wa Mungu kuvumbua  hazina zilizo ndani yake na kuzifanyia kazi na hapo ndipo kusudi la maisha linapokuwa limefikiwa. Zinahitajika jitihada za makusudi  na kukubali kujitoa dhabihu, kuwa tayari kupoteza kila kitu ili kusababisha  kuzaliwa na kile Mungu ameweka ndani yako.
Tazama mfano wa Ngano alioutoa Bwana wetu Ysu Kristo katika Injili ya Yohana  12:24

Amini, amini, nawaambia, chembe ya ngano isipoanguka  katika nchi,  ikafa, hukaa katika hali hiyo hiyo peke yake; bali ikifa hutoa mazao mengi.

Kumbuka Yesu Alisema ngano Isipokufa hubaki katika hali hiyohiyo, ni  lazima ngano ife ili iweze kumea na kuleta mazao mengi,  katika kanuni ya uzazi wa mimea tunajifunza  kuwa  ndani ya kifo hutoka maongezeko na mazidisho. Ni lazima ukubali kufa  katika kutimiza kile Mungu ameweka ndani yako. Hupaswi kujihurumia  hakuna mafanikio yasiyo na maumivu. Kubali kulipa gharama katika kuvumbua kile Mungu ameweka ndani yano na  uweze kusababisha kitokee kabla hujaondoka  duniani.

Hebu pitia   somo hili  ukiwa katika hali ya maombi, Mungu atakufunulia kweli yake takatifu kupitia somo hili. Nakuhakikishia kuwa utakapoamua kufanyia kazi kweli Mungu alizokufundisha kupitia somo hili  kamwe htabaki vile ulivyo.   Maisha yako na huduma yako itabadilika na kuwa katika viwango ulvyokusudiwa na  Mungu.
 Karibu tujifunze pamoja.

Myles Munroe ambaye ni kiongozi Mkristo alisema hivi kuhusu uwezo wa mwamini kufanya kitu katika kitabu chake kiitwacho Understanding Your Potential:
 “Mahali penye utajiri sana hapa duniani si katika maeneo ya mafuta huko Kuwaiti, Iraki au Saudi Arabia. Wala si katika machimbo ya dhahabu na almasi huko Afrika Kusini, au machimbo ya uranium huko Urusi au katika machimbo ya shaba yaliyoko Barani Afrika. Utashangaa tu lakini, utajiri mkubwa sana katika dunia yetu uko mita chache tu kutoka nyumbani kwako. Uko katika makaburi yenu. Huko chini, kumezikwa ndoto ambazo hazikuwahi kutimizwa, nyimbo ambazo hazikuwahi kuimbwa, vitabu ambavyo havikuandikwa, picha ambazo hazikuchorwa, mawazo ambayo hayakutolewa, maono ambayo hayakufanyika uhalisi, vitu vilivyobuniwa ambavyo havikutengenezwa, mipango ambayo haikutoka kwenye mawazo ya mtu na makusudi ambayo hayakutimizwa. Makaburi yetu yamejaa uwezo wa kufanya vitu ambao haukufanikiwa.
“Uwezo wa kufanya vitu unadai kwamba usikubali kutosheka na kitu ulichofanikisha. Adui mmoja ambaye ni mkubwa sana wa uwezo wako kufanya vitu ni mafanikio. Mafanikio kidogo huharibu uwezekano mkubwa! Ili uweze kufikia uwezo wako kamili wa kufanya vitu, hutakiwi kutosheka na ulichofanikisha. Pia ni muhimu kwamba usiruhusu kile usichoweza kufanya kiingiliane na kile unachoweza kufanya. Janga kuu maishani si kifo, bali ni maisha ambayo hayakufikia kilele chake katika uwezo wa kufanya vitu.
Katika kurahisisha dhana hii, hebu tutazame kitu kimoja katika uumbaji ambacho kina nguvu sana kitu hicho ni  mbegu.
 Nikishika mbegu mkononi na kuukuliza, ‘Nina nini mkononi?’ utasemaje? Pengine utajibu kilicho wazi kabisa   una  mbegu. Lakini, ukielewa asili ya mbegu, jibu lako linaweza kuwa uhalisi japo halitakuwa ukweli. Ukweli ni kwamba nimeshika msitu mkononi mwangu. Ni hivi: Katika kila mbegu kuna mti, na katika kila mti kuna matunda au maua yenye mbegu ndani yake. Na hizo mbegu nazo zina miti ambayo ina matunda yenye mbegu ndani yake   ambazo zina miti yenye matunda yenye mbegu, na kadhalika na kuendelea.
Unachokiona hapa si yote. Kwa hiyo, tofauti kati ya mbegu moja na utoaji wa chakula kama vile ngano inayoweza kulisha dunia nzima ni kitu kinachoitwa ‘uwezo wa kufanya vitu.’ Hicho ndicho kiwango cha tofauti kati ya unachoona na kinachowezekana
Kama Musa angekufa kabla hajaona kile kichaka kilichokuwa kinawaka moto au Paulo kabla ya kukutana na Yesu akiwa njiani kwenda Dameski  au Ibrahimu kabla ya Isaka kuzaliwa. Maandiko na historia vingekuwa tofauti sana. Kama Martin Luther angekufa bila ya kuandika  zile hoja zake (Thesis) au Charles Wesley bila ya kutunga nyimbo zake   au John Wycliff bila kufasiri Biblia katika lugha ya Kiingereza. Historia ya Kanisa ingekuwa tofauti sana.

 Sijui ingekuwaje kama baba yako angekufa kabla hujatungwa mimba, au mama yako kabla hujazaliwa. Dunia ingepoteza nini kama usingezaliwa? Je, dunia itakosa nini kwa sababu unashindwa kuishi kufikia kiwango cha uwezo wako wote? Je, utakwenda kaburini na nyimbo, vitabu, magunduzi au dawa?  

Je, inawezekana kwamba dhambi kuu ya Wakristo imo katika uwezo wao wa kufanya mambo ambao haujafikiwa? Tena, uwezo mkuu wa kufanya mambo ambao haujatumiwa katika siku za leo ni katika eneo la kutimizwa Agizo Kuu la Bwana wetu. Yeye amekupa wewe nafasi maalum katika Kuufikia Ulimwengu Kikamilifu, na ni   nafasi kubwa kuliko yoyote uliyowahi kuwa nayo. Hii nafasi haiwezekani bila ya maono kwamba inawezekana.
 Basi, kitu muhimu kuliko vyote katika maisha yako ni kuwa na maono yanayokubaliana na Mungu, na kuyafuatilia. Kwa kuwa kazi uliyopewa inahusu dunia nzima, maono yako lazima yawe hivyo hivyo. Je, una maono ya aina hiyo?
Sasa – watu kama wewe na mimi – wenye ubinafsi, kujijali, wenye kujali kwao na wenye kujiona wanapataje maono ya Mungu? Angalia kanuni hii, inayoweza kufanya kazi: habari sahihi ukijumlisha na kuangaziwa kiroho vitaleta maono, ambayo yatasababisha motisha, na hiyo motisha itapelekea utendaji wa kiroho wenye matokeo. Hapo, ona kwamba maono huanza kwa kupata habari sahihi. Sawa na ambavyo kuona kimwili kunavyoanza kwa kuwepo kwa kivutio cha nje, ndivyo na maono kiroho yanavyoanza kwa ukweli wa Mungu katika Maandiko na kila kitu ambacho kinahusiana na Maandiko.
 “Matofali” ya kujengea maono hayo ni: kufahamu Maandiko kiasi cha kutosha na moyo sikivu wa kusikia  sauti ya Mungu na kuitii, halafu ufahamu wa jiografia ya dunia na tamaduni za nchi mbalimbali, utambuzi kiroho wa matukio, maombi, kujisomea ili kupata habari, ujuzi binafsi (“njoo uone” katika Maandiko)   baadhi ya maeneo ya kimisheni duniani, ushirikiano na waamini wenye maono, kujitoa kwa ajili ya kutoa kuhusu mambo ya umisheni, kukutana na wamishenari na Wakristo wenye kugusa dunia, na maamuzi mbalimbali katika maisha. Unaweza kuanza kushirikiana na Mungu katika kujenga maono ya kiroho katika maisha yako leo. Lakini, ni dhahiri – na inasikitisha sana – kwamba Wakristo wengi unaoshirikiana nao mara kwa mara hawana maono kama hayo.
Omba Mungu  akupe kutambua kusudi la kuumbwa kwako kwa sababu hakuna mwanadamu aliyekuja kwa bahati mbaya katika dunia hii. Mungu anakusudi la kipekee na kila mtu.
Ninaamini kwamba ikiwa kila mtu angetimiza  walau hata kidogo  kusudi lake la kuwepo hapa duniani, dunia hii ingekuwa ya tofauti sana. Watu wengi wanaishi nje ya  makusudi yao ya kuwepo hapa duniani. Soma Neno la Mungu na    jenga utaratibu wa kuketi barazani pa  Mungu ili akusikizishe ili uweze kutambua kusudi lako la kuwepo hapa duniani na kutambua laslimali ambazo Mungu ameweka ndani yako na  namna unavyowea kutenda katika kutimiza kusudi lako. Kila mtu ni wa kipekee na ndani yake kuna vitu vya kipekee vinavyomfanya awe wa kipekee.
Tatizo kubwa  katika dunia ya sasa ni Maigizo. Watu wamekuwa wavivu   wa kugundua   hazina ambazo Mungu amaweka ndani yao na wamekuwa wakiiga vitu kutoka kwa watu wengine wanaodhani kuwa ni maarufu. Watu wamekuwa waigaji. Wahubiri wanaiga wahubiri wenzao, waimbaji wanaiga waimbaji wenzao nah ii imeleta ukasuku  katika huduma na katika maisha ya kawaida. Kuiga si kubaya  na  ila kunapochukua nafasi  na kusababisha mtu ashindwe kujifunza na kuvumbua hazina iliyoko ndani yake hap ndipo  kuiga kunapokuwa tatizo.
Tafuta kujua ni hazina zipi Mungu ameweka ndani yako na namna gani unaweza kuzifanya zikatokea, wawweza kuvumbua kwa njia zifuatazo:-  Soma Neno la Mungu, Soma Vitabu mbalimbali vilivyoandikwa  na watumishi wa Mungu na kisha kuwa na ushirika  wa kudumu na Mungu kwa njia ya Maombi, kuwa karibu na watumishi wa Mungu  kwaajili ya malezi yaani uwe na baba wa kiroho kwaajili ya malezi na maongozi.
Ni maombi yangu kwa Mungu  kwamba usife bila kutimiza kusudi mahususi la kuumbwa kwako. Usife bila kutoa mchango wako ambao Mungu ameuweka ndani yako. Dunia hii bado inasubiri mchango wako  kwani ni wa muhimu sana.

 Kwa mafundisho  zaidi piga simu Simu no. 0762532121/0765992774

Wako katika Mavuno ya Kiroho

_________________
Rev.Dr.  Erick L Mponzi
MKURUGENZI MKUU
ELAM CHRISTIAN HARVEST SEMINARY
 

No comments:

Post a Comment